Alhamisi 1 Januari 2026 - 19:00
Hijabu ni miongoni mwa vielelezo vya kujitolea kufuata amri za Mwenyezi Mungu

Hawza/ Jumuiya ya Kheri ya Al-Mabarrat iliandaa hafla katika Ukumbi wa Zahraa, uliopo ndani ya Jumuia ya Imamain Hasanayn (amani iwe juu yao) huko Haret Hreik, kwa ajili ya zaidi ya wasichana balehe 400 waliokuwa wamefikia umri wa kuwajibikiwa kisheria (taklifu ya kisheria).

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Kheri ya Al-Mabarrat iliandaa hafla katika Ukumbi wa Zahraa, uliopo katika Jumuia ya Imamain Hasnayn (amani iwe juu yao) huko Haret Hreik, kwa ajili ya zaidi ya wasichana balehe 400 waliokuwa wamefikia umri wa taklifu ya kisheria katika shule zao zilizopo Beirut.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na kusimamiwa na Hujjatul-Islam Sayyid Ali Fadlullah, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Beirut, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Muhammad Baqir Fadlallah, pamoja na kundi la wanazuoni wa dini, wanaharakati wa kijamii na kitamaduni, wakuu wa shule na familia za wasichana hao.

Baada ya kusomwa aya za Qur’ani Tukufu na kuimbwa wimbo wa taifa, wasichana waliobalehe waliingia ukumbini, na kundi la wanafunzi wa shule za Al-Mabarrat wakatumbuiza kwa nyimbo na maigizo yaliyochota maudhui yake kutoka katika dhana ya taklifu.

Kisha Hujjatul-Islam Fadlallah alitoa hotuba yake akisema: Leo kukutana nanyi ni furaha kubwa kwangu, katika mwezi huu mtukufu wa Rajabu, mwezi ambao Mwenyezi Mungu ameufanya kuwa mwezi wa utulivu, amani na matumaini, na katika mazingira yanayoambatana na kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtukufu Isa Ruhullah, pamoja na kuzaliwa kwa Bibi Aliyetukuka Fatima Zahra, Kiongozi wa wanawake wa walimwengu (amani iwe juu yake). Katika hali hii, tunayo heshima ya kushiriki furaha ya mabinti zetu katika kukubali jukumu ambalo Mwenyezi Mungu amewabebesha; jukumu ambalo mbingu, ardhi na milima zilishindwa kulibeba, lakini wao wamelikubali kwa uelewa, hiari na imani, na watalitekeleza kwa njia bora kabisa.

Aliongeza kusema: Jukumu hili ni kujitolea kufuata amri za Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza yaliyo wajibu na kuepuka yaliyo haramu, na hijabu ni miongoni mwa vielelezo vya kujitolea huku. Mabinti zetu kwa kuikubali, wamechagua kwa uelewa njia ya uongofu wa Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo njia bora ya maisha na mustakabali wao; njia inayohakikisha wokovu wao duniani na Akhera, kwani Mwenyezi Mungu hawatakii waja Wake ila kheri na maslahi, na hakuna amri wala katazo Lake isipokuwa kuamrisha mema na kuepusha maovu.

Hujjatul-Islam Fadlullah alisisitiza: Mabinti zetu wanafahamu kuwa Mwenyezi Mungu amewataka wajitokeze kama ishara ya ubinadamu wao, si kama maonesho ya kijinsia; na hakuna mahali popote—kuanzia mitaani na shuleni hadi vyuoni na sehemu za kazi—panapopaswa kuwa jukwaa la maonesho ya sura ya nje, bali ni uwanja wa kuonyesha nafasi na mchango hai wa mwanadamu muumini katika nyanja za kielimu, kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Beirut aliendelea kusema: Tunapozungumza kuhusu hijabu, hatumaanishi sura ya nje pekee, bali roho na maana yake inayodhihirisha kushikamana na amri ya Mwenyezi Mungu. Hijabu ni kinga ya akili ili ibaki mbali na mawazo potofu; ni kinga ya ulimi dhidi ya maneno ya kuumiza na yasiyofaa; ni kinga ya moyo dhidi ya chuki na husuda; na ni kinga ya nafsi ili ibaki katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mabinti zetu wanapaswa, kwa elimu, vitendo, maadili na ushiriki wao wenye tija katika jamii, kuwasilisha taswira nzuri zaidi ya maisha yenye afya na yenye imani, hususan katika uwanja wa kujenga taifa, uhuru wake na kujitegemea kwake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha